Taarifa Kwa Vyombo vya Habari- Japan na UNHCR zatia saini makubaliano ya $360,000 ili kusaidia wakimbizi wanaowasili Tanzania kutoka Kongo
Serikali ya Japan na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), leo zimetia saini makubaliano mapya ya ushirikiano utakaowezesha utoaji endelevu wa huduma muhimu ikiwemo malazi, maji safi na salama, na usafi wa mazingira, kwa wakimbizi wanaoendelea kuwasili mkoani Kigoma nchini Tanzania wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mchango wa dola za Kimarekani 360,000 kutoka kwa Serikali na watu wa Japan utasaidia kuimarisha huduma za dharura za kuokoa maisha kwa watu wanaokimbia machafuko nchini DRC.